Historia Fupi ya Maisha ya
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
Ayatullah Udhmaa Sayyid Ali Khamenei (daama dhilluh)
"Mtafuteni mtu mmoja mfano wa Sayyid Khamenei ambaye
ameshikamana barabara na Uislamu na ni mtumishi wa umma,
na ambaye amedhamiria kwa dhati ya moyo kulitumikia taifa hili,
muone kama mtampata mtu kama huyo aliye mfano wake yeye.
Mimi ninamjua yeye kwa miaka mingi."
Imam Khomeini (quddisa sirruh)
Tangu Kuzaliwa Kwake hadi Kuanza Masomo
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Udhmaa Sayyid Ali
Khamenei ni mwana wa marehemu Hujjatul Islam wal Muslimin al-Haj Sayyid Jawad
Husaini Khamenei. Alizaliwa katika mji mtakatifu wa Mashhad, tarehe 28 Safar
(Mfunguo Tano) mwaka 1358 Hijria, mwafaka na tarehe 18 Aprili 1939 Miladia. Yeye
ni mwana wa pili wa kiume katika tumbo lao. Maisha ya baba yake yaani Sayyid
Jawad Khamenei yalikuwa ya kawaida kabisa kama yalivyo ya wengi wa masheikh,
wanazuoni, na waalimu wa masomo ya dini. Mkewe na wanawe walijifunza mengi
mazuri kutoka kwake yeye mwenyewe mzee huyo, hasa juu ya maana halisi ya kukinai
na kutosheka pamoja na kuishi maisha yasiyo na makuu, kiasi kwamba sifa mbili
hizo zikawa ni miongoni mwa matendo yaliyopamba maisha yao ya kila siku.

Kiongozi Muadhamu anaelezea kumbukumbu za mwanzoni mwa maisha yake na jinsi
familia yao ilivyokuwa wakati huo, kwa kusema: ‘'Baba yangu alikuwa Sheikh
mashuhuri, lakini licha ya umashuhuri huo alikuwa mcha Mungu mno na mtu aliyeipa
mgongo dunia.... Tulikuwa tukiyapitisha maisha yetu ya kila siku kwa taabu na
mashaka. Bado ningali nakumbuka pale tulipokuwa tukipitisha usiku wa baadhi ya
masiku bila ya kupata mlo kamili wa usiku. Katika hali hiyo, mama yetu aliweza
kwa taabu na mashaka kututayarishia chakula cha usiku... na chakula chenyewe
basi kilikuwa ni mkate na zabibu kavu."
Kuhusu nyumba ilimokuwa ikiishi familia yake, Ayatullah Khamenei anauelezea
wasifu wake kwa kusema: ‘'Nyumba ya baba yangu nilimozaliwa na kuishi humo hadi
nilipofikisha umri wa miaka minne au mitano hivi, ilikuwa na ukubwa wa takriban
mita 60 hadi 70 katika mtaa wa watu masikini mjini Mashhad, ambayo ilikuwa na
chumba kimoja na kijichumba cha chini ya ardhi kilichokuwa na giza totoro!
Wakati baba alipokuwa akijiwa na mgeni (kwa vile alikuwa aalimu na marejeo ya
watu kutaaradhia shida zao ilikuwa ni kawaida kupata wageni mara kwa mara), sote
tulikuwa tukilazimika kwenda kwenye kijichumba cha chini ya ardhi na kubaki huko
hadi mgeni anapoondoka. Tuliendelea kuishi katika hali hiyo hadi pale baadhi ya
watu waliokuwa na mapenzi maalumu na baba, walipomnunulia kijiardhi kidogo kando
ya nyumba yetu kilichojengwa na kuunganishwa na nyumba yetu, na ndipo idadi ya
vyumba vya nyumba yetu ilipoongezeka na kufikia vitatu."
Hivi ndivyo alivyokulia; na kuanzia umri wa miaka minne yeye pamoja na kaka yake
Sayyid Muhammad walipelekwa chuoni kwa ajili ya kujifunza kuandika na kusoma
Quran. Baada ya hapo ndugu hao wawili walipelekwa kwenye madrasa ya kidini
ambayo ilikuwa ndio kwanza imeanzishwa wakati huo iliyokuwa ikiitwa
‘Daru-ttaalimi Diyanati' kwa ajili kupata elimu ya msingi ya mafunzo ya dini.
Katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza)
Baada ya kumaliza masomo ya sekondari ambako pia alisoma vitabu vya lugha na
sarufi ya Kiarabu, k.v. Jami'u 'l-Muqaddamaat, Sayyid Ali Khamenei alijiunga na
Hawza (chuo kikuu cha kidini) ambako alianza kujifunza kwa baba yake na walimu
wengine fasihi na masomo mengine ya kimsingi. Kuhusu kujiunga kwake na chuo cha
kidini anasema: "Baba yangu ndiye aliyekuwa sababu kuu ya mimi kuichagua njia
hii ya nuru ya kusomea taaluma za dini; na mama yangu naye pia alipendelea jambo
hilo na kunishajiisha pia".
Alisoma katika madrasa za Sulayman Khan na Nawwab, huku baba yake akiwa
anasimamia na kufuatilia masomo yake. Katika awamu hiyo alisoma pia kitabu cha
Ma'aalim. Kisha baada ya hapo akasoma kwa baba yake na pia kwa kiwango fulani
kwa marehemu Sheikh Mirza Mudarris Yazdi vitabu vya kifikihi vya vya Sharai'u
'l-Islam na Sharh al-Lummah. Aidha alisoma vitabu vingine vya kifikihi na
kiusuli, k.v. Rasa'il na Makasib kwa marehemu Sheikh Hashim Qazwini; na masomo
yaliyobakia ya usul na fikihi katika kiwango cha kati (sat'h) alisomeshwa na
baba yake. Ni jambo la kushangaza na lililo nadra sana kuona kwamba alifanikiwa
kukamilisha masomo yote ya shahada ya msingi (muqaddamaat) na ya kati (sat'h)
katika muda wa miaka mitano na nusu tu. Katika muda wake wote huo wa masomo,
baba yake, marehemu Sayyid Jawad alikuwa na nafasi muhimu katika maendeleo ya
mwanawe huyo hodari. Katika upande wa mantiki na falsafa, Sayyid Ali Khamenei
alisoma kitabu cha taaluma hizo cha Mandhumah cha Sabzwari, kwanza kwa marehemu
Ayatullah Mirza Jawad Agha Tehrani na baadaye kwa marehemu Sheikh Ridha Eisi.
Katika Hawza ya Najaf al-Ashraf
Akiwa na umri wa miaka 18, Ayatullah Khamenei alianza kuhudhuria darsa za
khariji (masomo ya juu kabisa) katika taaluma ya fikihi na usuli kwa marjaa
mkubwa wa wakati huo - Ayatullah Udhmaa Milani. Mnamo mwaka 1957, alifunga
safari ya kuelekea mjini Najaf al-Ashraf kwa ajili kuzuru maeneo matakatifu.
Baada ya kujionea mwenyewe na kushiriki pia katika darsa za khariji za mujtahidi
wakubwa wa Hawza ya Najaf akiwemo marehemu Sayyid Muhsin Hakim, Sayyid Mahmud
Shahrudi, Mirza Baqir Zanjani, Sayyid Yahya Yazdi na Mirza Hasan Bojnurdi,
Sayyid Ali Khamenei alivutiwa na kupendezwa na hali ya masomo hapo, mfumo wa
usomeshaji na uhakiki wake, hivyo akamjulisha baba yake nia yake ya kuendelea na
masomo huko, lakini baba yake hakukubaliana na wazo hilo. Hivyo, baada ya muda
akarejea Mashhad.
Katika Hawza ya Qum
Kuanzia mwaka 1958 hadi 1964 Ayatullah Khamenei aliendelea na masomo ya juu
kabisa ya fikihi, usuli na falsafa katika Hawza ya Qum na kufaidika na elimu za
maulamaa wakubwa wakubwa, k.v. marehemu Ayatullah Udhmaa Borujerdi, Imam
Khomeini, Sheikh Murtadha Haeri Yazdi na Allama Tabatabai. Mnamo mwaka 1964,
walipokuwa wakiandikiana barua, Ayatullah Khamenei aligundua kwamba jicho moja
la mzazi wake lilikuwa na mtoto, hivyo alihuzunika mno. Akiwa katika hali ya
njia panda baina ya kubaki Qum na kuendelea na masomo katika chuo muhimu cha
kidini cha mji huo na kurudi Mash-had kwa ajili ya kwenda kumtunza na kumhudumia
baba yake, mwishowe Ayatullah Khamenei alifikia uamuzi wa kurudi Mashhad kwa
ajili ya kumtunza na kumshughulikia baba yake. Akizungumzia kuhusu uamuzi wake
huo, Ayatullah Khamenei anasema: "Nilielekea Mashhad; na Mwenyezi Mungu Mtukufu
alinipa taufiki kubwa. Alakullihali nilikwenda huko kutekeleza wajibu wangu.
Kama kuna taufiki nimepata katika maisha yangu, naamini kwamba imetokana na wema
huo nilioufanya kwa baba yangu au niseme kwa wazazi wangu." Kwa hakika, katika
kuchagua moja kati ya njia mbili hizo, Ayatullah Khamenei alichagua njia sahihi
zaidi. Baadhi ya walimu na watu aliokuwa akijuana nao walikuwa wakisikitika kwa
nini aliamua kuondoka Qum mapema kiasi hicho, na kwamba laiti angebaki hapo,
angekuja kuwa hivi na vile kimafanikio katika mustakabali. Hata hivyo, baadaye
ilibainika kuwa uamuzi aliochukua ulikuwa sahihi, na kwamba takdiri ya Mwenyezi
Mungu ilikuwa imemwekea majaaliwa mengine na yaliyo bora zaidi ya yale
waliyokuwa wakifikiria wao. Je, kuna mtu aliyeweza hata kuwaza na kufikiria
kwamba katika enzi hizo aalimu huyo kijana mwenye kipawa akiwa na umri wa miaka
25, aliyeamua kwa sababu ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kuondoka Qum na
kurudi Mashhad ili kwenda kuwatunza na kuwashugulikia wazazi wake, miaka 25
baadaye angekuja fikia daraja ya juu ya kuwa kiongozi wa Umma wa Kiislamu?
Aliporudi Mashhad hadi mwaka 1969, Ayatullah Khamenei aliendelea kusoma fikihi
na usuli kwa maulamaa wakubwa wa Hawza ya Mashhad na hasa kwa Ayatullah Milani;
na hakusitisha masomo yake isipokuwa katika siku za mapumziko au zile alizokuwa
akijishughulisha na mapambano au alipokuwa safarini na kifungoni. Aidha kuanzia
mwaka 1964 ambapo aliamua kubaki rasmi huko Mashhad kwa ajili ya kusoma na
kumtunza baba yake ambaye alikuw amekwishakuwa mzee na mgonjwa, Ayatullah
Khamenei alijishughulisha pia na kuwasomesha wanafunzi wa masomo ya kidini na
wale wa vyuo vikuu vitabu vya kifikihi, kiusuli na mafunzo mengine ya dini.
Harakati za Kisiasa

Kama anavyoeleza mwenyewe, Ayatullah Khamenei ni miongoni mwa wanafunzi wa Imam
Khomeini (Allah amrehemu) katika masomo ya fikihi, usuli na vile vile harakati
za kisiasa na kimapinduzi. Hata hivyo, cheche ya kwanza ya harakati za kisiasa
na za mapambano dhidi ya taghuti ilipenya katika akili yake kupitia kwa mujahid
mkubwa na shahidi katika njia ya Uislamu, Shahid Sayyid Mujtaba Nawwab Safawi,
pale Nawab Safawi pamoja na idadi kadhaa ya wanamapambano wengine wa harakati za
Fadaiyane Islam walipokwenda Mashhad katika mwaka 1953 na kutoa hotuba kali ya
kusisimua na ya kimwamko katika madrasa ya Sulayman Khan juu ya maudhui ya
kuuhuisha Uislamu na utawala wa sheria za Mwenyezi Mungu, kubainisha hila na
hadaa za Shah na dola la kikoloni la Uingereza, na uwongo wao kwa wananchi wa
Iran. Ayatullah Khamenei ambaye siku hiyo alikuwa miongoni mwa vijana wanachuo
wa kidini aliathiriwa mno na hotuba kali ya Nawwab. Akizungumzia kuhusu hotuba
hiyo, anasema: "Pale pale cheche za hamasa ya kuleta mapinduzi ya Kiislamu
zilipenya ndani ya nafsi yangu kutokea kwa Nawwab Safawi, na sina shaka yoyote
kuwa marehemu Nawwab Safawi ndiye aliyewasha cheche ya kwanza ya mwamko ndani ya
moyo wangu."
Bega kwa Bega na Harakati za Imam Khomeini (quddisa sirruh)
Tokea mwaka 1962, wakati Ayatullah Khamenei alipokuwa katika mji wa Qum na pale
zilipoanza harakati za kimapinduzi na za upinzani za Imam Khomeini dhidi ya
siasa za kupiga vita Uislamu na kuikumbatia Marekani za Muhammad Reza Pahlavi,
aliingia kwenye uwanja wa mapambano ya kisiasa, ambapo licha ya taabu, mashaka,
mateso, kutupwa gerezani na kupelekwa uhamishoni, kwa muda wa miaka 16 kamili
aliendelea na mapambano katika njia hiyo bila ya kuhofu hatari yoyote. Kwa mara
ya kwanza katika Muharram ya mwaka 1959, Ayatullah Khamenei alipewa jukumu na
Imam Khomeini la kwenda kufikisha ujumbe kwa Ayatullah Milani pamoja na maulamaa
wengine wa Khorasan, juu ya namna ya kupanga mikakati ya kampeni
zitakazoendeshwa na maulamaa wakati wa mwezi wa Muharram za kufichua kwa
wananchi siasa za Shah za kujikumbatisha kwa Marekani na juu ya hali ya nchi
pamoja na matukio yaliyojiri Qum. Alitekeleza kazi hiyo aliyopewa, kisha yeye
mwenyewe akaelekea mji wa Birjand kwa ajili ya tablighi na kufikisha ujumbe wa
Imam Khomeini wa kufichua maovu ya utawala wa Kipahlavi na Marekani. Kwa sababu
hiyo, tarehe 9 Muharram sawa na tarehe pili Juni mwaka 1963, Ayatullah Khamenei
alitiwa nguvuni na kuwekwa rumande hadi siku ya pili yake ambapo aliachiwa huru
kwa sharti kwamba asije akapanda mimbari na kutoa hotuba, na pia awe akifatiliwa
nyendo zake. Kufuatia kujiri kwa tukio la Khordad 15 (Juni 5) Ayatullah Khamenei
aliondolewa Birjand na kupelekwa Mash-had, akakabidhiwa kwenye mahabusu ya
kijeshi na kuwekwa rumande kwa muda wa siku kumi huku akikabiliana na mazingira
magumu kabisa ya maudhi na mateso.
Kutiwa Nguvuni Mara ya Pili
Katika mwezi wa Januari mwaka 1964 (Ramadhan 1383), Ayatullah Khamenei pamoja na
wenzake kadhaa walipanga mkakati maalumu wa safari ya kuelekea Kerman. Baada ya
kusimama kwa siku mbili tatu huko Kerman na kuhutubia na kukutana na maulamaa na
wanafunzi wa kidini wa mji huo, waliendelea na safari yao hadi Zahedan. Hotuba
kali na za hamasa za Ayatullah Khamenei ziliwavutia wananchi, na hasa zile
alizotoa katika siku za kumbukumbu ya tarehe 26 Januari, siku ambayo ulifanyika
uchaguzi bandia wa kura za maoni uliopangwa na Shah. Tarehe 15 Ramadhani ambayo
ilisadifiana na siku ya kuzaliwa Imam Hasan AS, ushujaa, hamasa ya kimapinduzi
na ujasiri ulioonyeshwa na Ayatullah Khamenei wa kufichua siasa za kishetani za
Marekani na utawala wa Kipahlavi, zilifikia kilele chake kiasi kwamba usiku
huohuo alitiwa nguvuni na Savak (askari wa usalama) na kusafirishwa kwa ndege
hadi Tehran. Kwa muda wa karibu miezi miwili, Ayatullah Khamenei aliwekwa katika
seli ya peke yake kwenye jela ya Qezel Qal'eh na kukabiliana na kila aina ya
mateso na manyanyaso.
Kutiwa Nguvuni Mara ya Tatu na ya Nne
Darsa zake za tafsiri ya Qur'ani, hadithi na fikra za Kiislamu katika miji ya
Mashhad na Tehran zilihudhuriwa kwa wingi mno na vijana wengi waliokuwa na
hamasa kubwa ya kimapinduzi. Harakati zake hizo ziliwaghadhibisha Savak na hivyo
wakaanza kumfuatilia. Kutokana na hali hiyo, katika mwaka 1967 Ayatullah
Khamenei akawa anaishi kwa kujificha katika mji wa Tehran, na mwaka mmoja
baadaye, yaani mwaka 1968, alitiwa nguvuni na kuwekwa korokoroni. Harakati hizo
za kielimu na uwekaji vikao, usomeshaji na utoaji hotuba za kuiamsha na
kuirekebisha jamii, ndizo zilizopelekea mnamo mwaka 1971 akamatwa tena na kikosi
cha usalama (Savak) cha utawala wa Shah na kutiwa jela.
Kutiwa Nguvuni Mara ya Tano
Akizungumzia kutiwa nguvuni kwake kwa mara ya tano na Savak, Ayatullah
Khamenei (Allah ampe umri) amesema: "Kuanzia mwaka 1970, mazingira ya kuanzishwa
harakati za mtutu wa bunduki yalianza kuhisika nchini Iran. Harakati za vyombo
vya utawala wa wakati huo za kunifuatilia mimi zilikuwa kubwa mno na zikazidi
kuongezeka kwa sababu vilihisi kwamba haingewezekana kuwepo harakati kama hizo
bila kuwa na mahusiano na watu kama mimi. Mwaka wa 1971 na kwa mara ya tano
nilitiwa jela tena. Vitendo vya kikatili vilivyokuwa vikifanywa na Savak huko
jela, vilionyesha dhahiri kuwa vyombo vya dola vilikuwa na hofu kubwa ya
kuungana harakati za mapambano ya silaha na zile za fikra za Kiislamu, na
havikuwa tayari kukubali kwamba harakati zangu za kifikra na kitablighi za
Mashhad na Tehran hazikuwa na mfungamano na harakati hizo. Baada ya kuachiwa
huru, wigo wa darsa zangu za tafsiri kwa watu wote na zile za siri za masuala ya
kiitikadi zilizidi kuongezeka."
Kutiwa Nguvuni Mara ya Sita
Kati ya mwaka 1971-1974 darsa za tafsiri ya Qur'ani na masuala ya kiidiliojia
(kiitikadi) za Ayatullah Khamenei zilikuwa zikifanyika katika misikiti mitatu:
Karamat, Imam Hasan AS na Mirza Jaafar huko Mashhad na kuvutia watu wengi hasa
vijana waelewa, walioamka kifikra, na wanafunzi wanamapinduzi wa kidini ambao
walipata fursa ya kuelewa fikra sahihi za Kiislamu. Darsa zake za Nahju
'l-Balagha, nazo pia zilikuwa na msisimko na hali ya aina yake, na zikawa
zinachapishwa na kukathiriwa na mashine ya kurudufia kwa jina la "Nuru kutoka
kwenye Nahju 'l-Balagha" na kusambazwa mkono mwa mkono. Wanafunzi vijana
wanamapinduzi wa kidini ambao walikuwa wakisoma kwa Ayatullah Khamenei darsa juu
ya ukweli na mapambano, walikuwa wakielekea kwenye miji ya mbali na karibu ya
Iran kuziamsha fikra za wananchi kwa kuwaelimisha juu ya masuala hayo na
kutayarisha mazingira kwa ajili ya mapinduzi makubwa ya Kiislamu.
Kwa sababu ya harakati hizo, mnamo mwezi Disemba mwaka 1974, Savak walivamia
nyumba ya Ayatullah Khamenei huko Mashhad wakamtia nguvuni na kukamata pia
kumbukumbu na maandishi yake mengi. Hiyo ilikuwa ni mara yake ya sita kutiwa
nguvuni na kukabiliwa na hali mbaya zaidi. Aliendelea kuwekwa kwenye jela ya
makao makuu ya polisi hadi msimu wa mapukutiko wa mwaka 1975 . Katika kipindi
hicho cha kuweko korokoroni aliwekwa kwenye seli yenye hali mbaya mno. Mateso na
shida alizozipata katika wakati huo alipotiwa nguvuni kwa mara ya sita, ni kama
anavyoeleza mwenyewe kwamba: "Wanaoweza kuyaelewa hasa ni wale tu waliowahi
kufikwa na hali hiyo." Baada ya kutolewa jela, alirejea kwenye mji mtakatifu wa
Mashhad na kuendelea na ratiba zake zilezile za utafiti wa kielimu na harakati
za kimapinduzi. Hata hivyo hakupewa fursa tena ya kuendesha darsa zake kama
ilivyokuwa zamani.
Uhamishoni
Mwishoni mwa mwaka 1977, utawala wa kinyama wa Kipahlavi ulimtia nguvuni
Ayatullah Khamenei na kumpeleka uhamishoni kwa muda wa miaka mitatu huko kwenye
mji wa Iranshahr. Katikati ya mwaka 1978 wakati harakati za mapambano ya
wananchi Waislamu na wanamapinduzi wa Iran zilipokuwa zimepamba moto, Ayatullah
Khamenei aliachiwa huru huko uhamishoni na hivyo kurejea mjini Mashhad ambako
alijiunga kwenye safu ya mbele ya mapambano ya wananchi dhidi ya utawala katili
wa Kipahlavi. Mwishowe, baada ya miaka 15 ya mapambano ya kishujaa, jihadi na
subra katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kuvumilia kila aina ya taabu, shida na
machungu, aliyashuhudia matunda ya mapambano hayo, ambayo yalikuwa ni ushindi wa
mapinduzi makubwa ya Kiislamu ya Iran na kuanguka kiidhilali kwa utawala wa
kidhalimu wa Kipahlavi na kusimamishwa utawala wa Kiislamu katika ardhi ya Iran.
Karibu na Ushindi wa Mapinduzi

Wakati ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulipokuwa unakaribia, kabla ya Imam
Khomeini (quddisa sirruh) kurejea nchini kutoka Paris (Ufaransa), kiongozi huyo
aliunda Baraza la Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran lililoshirikisha shakhsia
wanamapambano kama vile Shahid Mutahhari, Shahid Beheshti, Hashemi Rafsanjani na
wengineo. Kwa amri ya Imam Khomeini, Ayatullah Khamenei akawa ni miongoni mwa
wajumbe wa baraza hilo. Ujumbe wa Imam Khomeini wa kumteua kuwa mjumbe wa baraza
hilo alifikishiwa Ayatullah Khamenei na Shahid Mutahari (r.a), na baada ya
kupokea ujumbe huo wa kiongozi mkuu wa Mapinduzi aliondoka Mashhad na kuelekea
Tehran.
Baada ya ushindi wa mapinduzi ya kiislamu, Ayatullah Khamenei aliendelea kwa
hamu, shauku na raghba kubwa na harakati za Kiislamu na kubeba majukumu
mbalimbali ili kuhakikisha malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu yanafikiwa; majukumu
ambayo kila moja na katika wakati wake lilikuwa na athari ya kipekee na umuhimu
mkubwa mno. Majukumu na nyadhifa hizo katika mfumo wa jamhuri ya Kiislamu ya
Iran tunazitaja hapa kwa muhtasari:
• Kuasisi Chama cha Jamhuri ya Kiislamu (Hizb-e Jamhoriy-e Islami) mnamo mwezi
Machi mwaka 1979 kwa ushirikiano wa wanazuoni wanamapambano wenzake kama vile
Shahid Beheshti, Shahid Bahonar, Hashemi Rafsanjani, n.k.
• Naibu Waziri wa Ulinzi, mwaka 1980.
• Msimamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah), mwaka 1980.
• Imam wa Sala ya Ijumaa ya Tehran, mwaka 1980.
• Mwakilishi wa Imam Khomeini (quddisa sirruh) katika Baraza Kuu la Ulinzi,
mwaka 1981.
• Mbunge wa wananchi wa Tehran katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge),
mwaka 1980.
• Mnamo mwezi Septemba mwaka 1980 pale vilipoanza vita ilivyotwishwa Iran na
Iraq, aa jeshi la Saddam kushambulia mipaka ya Iran kwa uchochezi na misaada ya
silaha ya madola makubwa na ya kishetani yakiwemo ya Marekani na Urusi ya
zamani, Ayatullah Khamenei akiwa amevalia sare za kijeshi alijiunga kwenye
medani za vita vya kujitetea kutakatifu.
• Tarehe 27 Juni mwaka 1981 alijeruhiwa vibaya katika jaribio la kutaka kumuua
lililofanywa na wanafiki kwa kutega bomu wakati akihutubia ndani ya msikiti wa
Abu Dharr mjini Tehran
• Kufuatia kuuawa shahidi Muhammad Ali Rajai, Rais wa pili wa Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran mnamo mwezi Septemba mwaka 1981, Ayatullah Khamenei
alichaguliwa kwa kura zaidi ya milioni kumi na sita na kupewa hukumu ya
kuidhinishwa rasmi kuwa Rais na Imam Khomeini (quddisa sirruh). Alichaguliwa
tena kwa mara ya pili kuwa Rais na kushika wadhifa huo kutoka mwaka 1985 hadi
mwaka 1989.
• Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Utamaduni, mwaka 1981.
• Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo (wa Kiislamu), mwaka
1987.
• Mwenyekiti wa Baraza la Kuipitia Upya Katiba, mwaka 1989.
• Mnamo tarehe 4 Juni mwaka 1989, na kufuatia kuaga dunia Kiongozi Mkuu wa
Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini (quddisa sirruh), Ayatullah Khamenei
alichaguliwa na Baraza la Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi, kuwa Kiongozi Mkuu na
Fakihi Mtawala. Uteuzi huo ulikuwa sahihi na wenye baraka kwani baada ya kuaga
dunia Imam Khomeini, Ayatullah Khamenei ameweza kwa mafanikio makubwa kuuongoza
Umma wa Kiislamu wa Iran bali pia Umma wa Kiislamu duniani.
Uandishi na Utafiti
1. Nadharia Jumla ya Fikra za Kiislamu katika ya Quran
2. Katika Kina cha Sala
3. Mazungumzo kuhusu Subira
4. Vitabu Vinne Vikuu katika Elimu ya Rijali
5. Utawala (Wilayat)
6. Ripoti Kuhusu Historia na Hali ya Sasa ya Hawza ya Mashhad
7. Wasifu wa Maimamu wa Kishia (Hakijachapishwa)
8. Viongozi Wakweli
9. Umoja na Uundaji Vyama
10. Sanaa kwa Mtazamo wa Ayatullah Khamenei
11. Ufahamu Sahihi wa Dini
12. Nafasi ya Mapambano Katika Maisha ya Maimamu AS
13. Roho ya Tawhidi: Kutomwabudu Asiyekuwa Allah
14. Haja ya Kurejea kwenye Qur'ani
15. Sira ya Imam Sajjad AS
16. Imam Ridha AS na Urithi wa Ukhalifa
17. Hujuma za Kiutamaduni (Mkusanyiko wa Ujumbe na Hotuba za Kiongozi Muadhamu)
18. Hadithi ya Wilayat (Mkusanyiko wa Ujumbe na Hotuba zake ambazo hadi sasa
zimeshachapishwa katika juzuu 9), n.k.
• Tarjuma
1. Suluhu ya Imam Hasan AS, kimeandikwa na Radhi Aal Yasin
2. Mustakabali katika Ulimwengu wa Uislamu, kimeandikwa na Sayyid Qutb
3. Waislamu Katika Harakati za Ukombozi wa India, kimeandikwa na Abdul Mun'im
Namri Nasri
4. Hati ya Mashtaka Dhidi ya Ustaarabu wa Magharibi, kimeandikwa na Sayyid Qutb